Kenya na Marekani wamezindua awamu ya pili ya mazungumzo ya kibiashara, siku chache tu baada ya kinyang’aniro cha uchaguzi huko Marekani. Inazingatiwa kuwa Marekani haijatia sahihi mikataba kama ile ya Basel na ya Paris ambayo inadhibiti usafirishaji wa taka za plastiki na udhibiti wa hali ya anga mtawalia. Ukosefu wa Marekani kuonyesha uongozi katika mikataba hii ya kimataifa ni dhahiri kwamba watakapoenda katika haya mazungumzo, watatumia mbinu kuwashawishi wenzao wa Kenya kulegeza misimamo yao na sheria zao za kimazingira. 

Nchi za kanda ya Afrika mashariki ambazo zimekuwa zikiweka mikakati ya kuungana kiuchumi na kibiashara zimegadhabishwa sana na mashauriano haya. Miezi mitatu iliyopita, makampuni ya Kimarekani ya plastiki na kemia yamekuwa yakimshurutisha mshirikishi wa mazumngumzo ya kibiashara wa Marekani kuyatumia kama mbinu ya kuingiza bidhaa za plastiki na kemia ndani ya Africa. Wanaashiria kwamba Ke nya itakuwa muundo msingi ama mfano wa mazungumzo ambao utatumika katika nchi zengine za bara la Afrika. Kufikia sasa, Marekani bado hawajaamua ni nchi zipi ambazo watafanya mazungumzo ya aina hii. 

Hili ni jambo ambalo limeleta tumbo joto kwa wakaazi wa bara la Afrika, na kulingana na ripoti kwenye mitandao ya jamii, mashirika yasiyo ya kiserikali, vyombo vya habari na kwenye uma, mazungumzo haya huenda yakadhalilisha sheria za kimazingira kama udhibiti wa plastiki ambazo Kenya na nchi zingine za Afrika zimepitisha. 

Mpangilio huu unaashiria kutumia mazungumzo haya kama mbinu ya kuhakikisha kwamba kampuni hizi zinaweza kufungua soko la bidhaa hizi kwa njia tofauti. Njia ya kwanza ni kuhakikisha kwamba Kenya inafungua uwekezaji wa viwanda hivi kwa muundo, mbinu ambayo inatoa vikwazo vilivyowekwa kuzuia bidhaa za plastiki. Vikwazo vingine ambavyo vinaweza kuzuia wawekezaji ni ushuru unaolipiwa bidhaa za kemia na plastiki. Ushuru huu ambao uko kwa kiwango cha juu umewekwa kuhakikisha kwamba wawekezaji wa nchi za kigeni waweze kutumia sarafu za kigeni. Mbinu nyingine ni kutumia vipengele vya kisheria ambavyo vinaruhusu nchi kufungua mipaka kwa bidhaa za kimarekani ni kutoza ushuru. Mbinu ya tatu, ni kutumia uwekezaji wa kibiashara ili kuruhusu wawekezaji wa kampuni hizi kuweka viwanda katika bara la Afrika. 

Cha msingi ni kuzingatia sera ambazo Kenya na nchi zingine thelathini na nne zimeweka kuzingiti utumizi mbaya wa mifuko na bidhaa za plastiki ambazo kwa undani zimedhuru mazingira hususan mito, maziwa, kwenye miji na vitongoji  vinginevyo. Ili kukabidiana na changamoto hii, shirika la Greenpeace  limekuwa katika mstari wa mbele kuhimiza wizara husika ya biashara na viwanda kuchukua hatua dhabiti na kuhimiza Marekani kuondoa vipengele hivi ambayo vinaweza kushusha hadhi ya kimazingira nchini Kenya na bara la Afrika.

Nakala asili ilichapishwa katika gazeti  la Taifa leo.

Fredrick Njehu, shirika la Greenpeace Africa

Plastic Clean Up and Brand Audit Activity in Africa. Get Involved